Na Teresia Mhagama, Dar es Salaam
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuhakikisha kuwa uwekaji wa vinasaba kwenye mafuta kama vile petroli na dizeli unafanyika kuanzia kwenye matenki yanayohifadhi mafuta hayo badala ya magari ili kuhakikisha kuwa mafuta yote yanayosambazwa nchini yanakuwa na ubora na Serikali inapata kodi stahiki.

Dkt.Kalemani alitoa agizo hilo tarehe 28 Aprili, 2021 mara baada ya kufanya ziara kwenye maghala ya mafuta ya kampuni za Camel Oil na Oil Com, Kurasini mkoani Dar es Salaam na kukuta wataalam kutoka TBS wakifanya kazi ya uwekaji wa vinasaba kwenye magari ya kusafirisha mafuta ya kampuni tajwa.

“Nataka muanze kupima mafuta kuanzia kwenye matenki yenyewe, hadi kwenye vituo, siyo tu kusubiri pale wanapopakia kwenye magari, Je ikitokea wamepakia wakati hampo, mtajuaje kuwa mafuta husika yana ubora?”Alisema Dkt.Kalemani

Dkt.Kalemani alieleza kuwa, amefanya ukaguzi wa kazi ya uwekaji wa vinasaba kwenye mafuta ili kujiridhisha kama TBS wanafanya kazi husika kwa ufanisi baada ya kukabidhiwa kutekeleza jukumu hilo ambalo awali lilikuwa likifanywa na mkandarasi binafsi ambaye alikuwa akilipwa takriban shilingi Bilioni Tano kwa mwezi.

Aliongeza kuwa, Serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi kumlipa mkandarasi binafsi kuweka vinasaba kwenye mafuta badala ya TBS ambayo ndiyo yenye dhamana ya kuhakikisha kuwa mafuta yanayouzwa nchini yanakuwa na ubora stahiki.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa, mafuta yanakuwa na ubora, kodi zinapatikana na pia tunajenga uwezo wa watu wetu kufanya kazi husika na Taasisi zetu zisimamie kazi hii badala ya kutegemea watu kutoka nje ya nchi.” Alisisitiza Dkt.Kalemani

Katika ukaguzi huo, Dkt.Kalemani aliiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), kuhakikisha kuwa, wanasimamia kikamilifu kazi ya uwekaji wa vinasaba kwenye mafuta nchini kwani TBS ina jukumu la kupima mafuta hayo na EWURA ndiye mwenye jukumu la kumsimamia mpimaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Athuman Ngenya alimhakikishia Waziri wa Nishati kuwa, TBS ina uwezo wa kufanya kazi ya uwekaji vinasaba kwenye magari na kwamba mafuta yote yanayosambazwa nchini yanakuwa na vinasaba.

Katika ziara yake kwenye maghala hayo ya mafuta mkoani Dar es Salaam, Waziri wa Nishati aliambatana na Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi, Sebastian Shana, na Wakuu wa Taasisi za Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), TBS na EWURA.