Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe: Jenista Mhagama, ametoa maagizo kwa menejimenti ya ofisi hiyo ili kuboresha  utendaji kutokana na mabadiliko yaliyofanyika ndani ya ofisi hiyo.

Kwa sasa majukumu ya ofisi hiyo ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu yamekuwa yakisimamiwa na Katibu Mkuu mmoja na Manaibu Makatibu Wakuu wawili, awali walikuwepo Makatibu Wakuu wa tatu kwa kila mmoja akisimamia majukumu yake.

Kabla ya kutoa maelekezo hayo kwenye kikao kazi na menejimenti ya ofisi hiyo kilichojumuisha wakuu wa idara, vitengo na taasisi zilizo chini ya ofisi hiyo leo tarehe 9 Aprili, 2021 Jijini Dodoma, Waziri Mhagama amebainisha kutoridhishwa na baadhi ya watendaji kutoshiriki kikamilifu kwenye kikao cha Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa masuala kama ilivyotakiwa na mkaguzi huyo.

“Kila tunachofanya ni kwa ajili ya taswira ya ofisi ya  Waziri Mkuu,  nasikitika mingoni mwetu tukishindwa kutekeleza wajibu wetu tutatia doa ofisi ya Waziri Mkuu. Katibu mkuu fikiria utaratibu wa kudhibiti uzembe lazima kila mmoja awajibike. Tumepanga katika mambo ya msingi hatutasita kufuatilia utendaji ili kila mmoja atokomeze wajibu wake.”amesema Mhe. Mhagama.

Akitoa maagizo katika kikao hicho amewataka watumishi kutanguliza taifa kwa kila jambo pia na kuwa wazalendo katika kutekeleza majukumu yao. Aidha amewataka kutumia ubobezi wa  taaluma walizo nazo ili kuleta matokeo chanya kwenye ofisi hiyo sambamba na kuwa wabunifu katika  utendaji wa shughuli zao.

Aidha Mhe. Mhagama ameagiza kufanyika kwa  vikao vya kila robo muhula ili kujipima na kutathimini namna ya utendaji wa shughuli za idara na taasisi za ofisi hiyo,alisisitiza vikao hivyo vitaweza kuchangia kuleta mabadiliko ya haraka ya kiutendaji katika idara zote na kupata matokeo yaliyo kusudiwa.

Pia,  Waziri Mhagama amezitaka Idara na Taasisi zilizo chini ya  ofisi hiyo kueandeleza dhana ya mshikamano katika utekelezaji wa shughuli ya ofisi ya waziri mkuu, amelieleza mafanikio ya moja ya idara ya ofisi hiyo  ni mafanikio ya ofisi nzima hivyo amewataka watumishi wote kushirikiana.

Mhe. Mhagama ameagiza kuhakikisha Mabaraza ya wafanyakazi katika ofisi hiyo yaendelee kufanyika.Aidha,  amesisitiza kuhakikisha katika idara,wizara  na tasisi za serikali  pamoja na sekta binafsi mabaraza hayo yanafanyika ili  waweze kuimarisha uhusiano kati ya waajiri na wafanyakazi.

Aidha, Waziri Mhagama ameagiza kabla ya mwisho wa mwezi huu, mfumo wa kielektroniki wa vibali vya kazi na ukaazi kwa wageni  uwe umezinduliwa na kufanya kazi ili kudhibiti mianya ya rushwa. Mfumo huo utasaidia kupunguza urasimu wa utoaji vibali kwa wawekezaji.

“Tayari tumesha wafukuza baadhi ya maafisa kazi wanye tabia ya kupokea rushwa kwenye vibali, tunataka mfumo huo kusaidia kutoa rushwa kwenye vibali, tunazo taarifa sisi tukisha pitisha utoaji vibali hivyo vinachukua zaidi ya wiki mbili havijatolewa ili kumfikia muhusika. Nataka mfumo huo uanze kufanya kazi.” Amesema Mhe. Mhagama.

Pia waziri ameagiza kukutanishwa na maafisa rasilimali watu kutoka kwenye makampuni makubwa ya uwekezaji nchini ili waelezwe utaratibu sahihi wa utoaji vibali, amefafanua kwamba baadhi ya mawakala wanawowasaidia makampuni hayo katika kupata vibali hivyo wamekuwa wakikiuka taratibu hivyo baadhi wamechukuliwa hatua. Aidha ameagiza kuhakikisha kuwa mikataba ya ajira inatolewa na wajiri nchini pamoja na kuzingatia mishahara wanaoyo lipwa.

Pia ameagiza  kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi kuwepo na “Labour Clinic” ya kushughulikia kero  na malalmiko ya wafanyakazi, waajiri na   wadau wengine katika sekta ya kazi na ajira.

“Nilizindua Mpango kazi wa Kushughulikia Malalamiko na Kero za Wafanyakazi, Waajiri na Wadau wengine kwenye sekta ya Kazi na Ajira Februari 29 mwaka huu Mkoani Morogoro lengo ikiwa kushughulikia kwa urahisi matatizo ya wadau hao, sijapata ripoti yoyote ya kujua labour clinic hizo zinaendelea hivyo naagiza zitekelezwe.

Pamoja na hayo ameagiza kufanyika ukaguzi kwenye makampuni na migodi, miradi ya kimkakati na makampuni mengine mbalimbali, alisema kuwa ukaguzi huo utasaidia kuwanufaisha watanzania kuwa na uwiano wa ajira pamoja na mishahara.

“Natambua tupo kipindi cha mpito cha kubadili mifuko ya hifadhi ya jamii nataka ndani ya wiki moja Katibu Mkuu hakikisha vikao vya kimkakati tulivyo viweka kwa kushirikiana vyama vya waajiri, vyama vya wafanyakazi na sisi serikali vinanza kufanyika ili zoezi hilo liweze kukamilika kama lilivyo agizwa,” amesisitiza Mhe. Mhagama.

Masuala mengine ambayo ameagiza Waziri Mhagama ni kufuatilia mradi wa kukuza ujuzi, mafunzo ya uwanagenzi, mafunzo kwa vitendo mahali pa kazi kwa wahitimu, suala la migogoro kwa wafanyakazi kupitia tume ya usuluishi na uwamuzi, masuala ya mawakala kukagua mahali pa kazi. Pia ameitaka Kitengo cha Huduma za Ajira kushirikiana na Uhamiaji na Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika kuibua ajira zenye staha nje ya nchi na makubaliano kuangaliwa upya ya ajira hizo.

Aidha,   ameelekeza utekelezaji wa maagizo yake kwenye mradi wa Mkulazi 1 na Mkulazi 2 aliyoyatoa bado hayajatekelezwa, hivyo ameagiza kukutana na timu ya wataalam wa NSSF wanaoshughulikia miradi hiyo pia ameelekeza kukutana na maafisa matekelezo (Compliance Officers) na Mameneja wa Mkoa wa mfuko wa hifadhi ya jamii NSSF.

Sambamba na hayo amesisitiza umuhimu wa ujumuishwaji wa masuala ya Watu wenye ulemavu katika kila nyanja pia kuhakikisha hata sekta nyingine zinatambua mchango wa watu wenye ulemavu katika kukuza maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajiara na Wenye Ulemavu) Tixon Nzunda, amemhakikishia Waziri Mhagama kutekeleza Maagizo yote  kwa kuzingatia misingi ya weledi, Uadilifu, bidii ya kazi ili kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa kwa wakati.