Watumishi Wa Umma Tumieni Jitihada Binafsi Kutoa Huduma Bora Kwa Wananchi
Na. Veronica Mwafisi-Dodoma
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Watumishi wa Umma nchini kutumia jitihada binafsi katika kutekeleza majukumu yao ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akiwa kwenye ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Mhe. Ndejembi amesema ni vema Watumishi wa Umma wakatathmini mchango wao binafsi katika Utumishi wa Umma ili waweze kuwa na tija katika utoaji wa huduma kwa umma.
“Ukiwa Mtumishi wa Umma uliyejitoa kuwahudumia Watanzania unapaswa kujiuliza unataka kufanya nini ili kutimiza malengo yako na ya Taasisi kwa ujumla,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Kuhusiana na madai mbalimbali ya kiutumishi, Mhe. Ndejembi amewaambia watumishi hao kuwa, wakati Serikali inayafanyia kazi madai yao ni vema wakatekeleza wajibu wao kikamilifu ili madai yao yawe na thamani inayolingana na huduma wanayoitoa.
Aidha, amewasisitiza Wakuu wa Idara na Vitengo katika Taasisi za Umma kuwasilisha mpango kazi kwa Watendaji Wakuu wa Taasisi zao utakaoziwezesha Idara na Vitengo pamoja na Taasisi kutekeleza majukumu kikamilifu.
Katika kuhimiza uwajibikaji unaozingatia maadili ya kiutumishi, Mhe. Ndejembi amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Wilaya ya Chamwino Bw. Athman Masasi, kumpa barua ya onyo Mpima Ardhi wa Halmashauri hiyo, Bw. Charles Laseko kwa kosa la kushinikizwa na Afisa Usalama kuweka alama ya mpaka kwenye Kiwanja ambacho kimeuzwa na Jiji kwa mtu mwingine.
Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma.