Mahakama ya Uturuki imewahukumu wanajeshi 32 wa zamani kifungo cha maisha jela kwa kuhusika katika jaribio la mapinduzi lililoshindwa la mnamo mwaka 2016 lililonuiwa kumuondoa madarakani rais Recep Tayip Erdogan. 

Hayo ni kwa mujibu wa wakili wa mmoja wa wanajeshi hao. Katika kesi ya hivi karibuni mahakama ya mjini Ankara ilichunguza jukumu la wanajeshi wa zamani 497, wakiwemo wa kikosi cha ulinzi wa rais. 

Hukumu hiyo imesomwa katika chumba kikubwa kabisa cha mahakama iliyojengwa mahususi kusikiliza kesi za jaribio hilo la mapinduzi katika gereza la Sincan mkoani Ankara. Kesi dhidi ya kikosi hicho ilianza kusikilizwa mnamo mwezi Oktoba mwaka 2017. 

Jaribio la mapinduzi lilisababisha vifo vya watu 248, mbali na waliohusika na ajribio la mapinduzi waliouliwa usiku wa tukio. 

Uturuki inamtuhumu shehe wa kiislamu ananyeishi uhamishoni Fethullah Gulen kwa kupanga jaribio hilo la mapinduzi, madai ambayo anayakanusha.