Na. James K. Mwanamyoto
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Watumishi wa Ofisi yake kusimamia utekelezaji wa ahadi za masuala ya kiutumishi na utawala bora zilizoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020 ili kuhakikisha Sekta ya Umma inaimarika na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi yake uliofanyika jijini Dodoma.

Mhe. Ndejembi amelitaka baraza hilo kupitia na kuchambua Ilani kwa kina na kubaini ahadi zinazohusu Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kwa ufanisi mkubwa ili kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.

Akihimiza utekelezaji wa Ilani katika Taasisi za Umma, amewataka Watumishi wa Umma kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na weledi ili kuiwezesha Serikali kutekeleza ahadi ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mhe. Ndejembi amesema, licha ya Watumishi wa Ofisi ya Rais-Utumishi kufanya kazi kwa weledi katika kutekeleza Ilani, lakini wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanabadili mtazamo hasi dhidi yao kwani malalamiko mengi yanayowasilishwa Utumishi yanatokana uzembe wa Watumishi wa Taasisi nyingine.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wajumbe wa baraza, Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Sera, Bi. Agnes Meena amemuahidi Mhe. Ndejembi kuwa, Utumishi itahakikisha inaishauri vizuri Serikali kutekeleza Ilani na kuongeza kuwa, watumishi wataendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuiwezesha ofisi kufikia malengo yake.

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imefanya kikao cha Baraza la Wafanyakazi kwa mujibu wa sheria, ambapo Taasisi za Umma zinapaswa kukutana kupitia mpango na bajeti itakayowasilishwa Bungeni, kabla Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania halijapitisha bajeti husika kwa ajili ya utekelezaji.