Urusi imewaamuru wanadiplomasia 20 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Czech na kuwapa muda wa siku moja kuondoka mara moja nchini humo.

Hilo ni jibu kwa serikali ya Jamhuri ya Czech kwa kuwafukuza wanadiplomasia 18 wa Urusi iliyowataja kuwa majasusi wa kijeshi na ambao serikali mjini Prague inadai walihusika kwenye shambulizi la kiwanda chao cha silaha mwaka 2014.

Balozi wa Jamhuri ya Czech Vitezslay Pivonka aliamriwa kufika katika wizara ya mambo ya nchi za nje ya Urusi jana Jumapili na kuarifiwa kuwa wanadiplomasia 20 wao waondoke nchini humo ifikapo jioni ya leo.

Mapema jana wizara hiyo ilitoa taarifa ikishutumu hatua ya Czech kuwatimua wanadiplomasia wa Urusi na kuitaja kama hatua ya uhasama.