Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya imesema kwamba imeanzisha mchakato wa kisheria dhidi ya kampuni ya AstraZeneca kwa kushindwa kuheshimu makubaliano ya kusambaza chajo dhidi ya virusi vya corona na kukosa mpango wa kuaminika wa kuhakikisha mgawo huo unafanyika kwa muda uliopangwa. 

Msemaji wa halmashuri hiyo Stefan De Keersmaecker amesema walianza mchakato huo Ijumaa iliyopita. 

Amewaambia waandishi habari mjini Brussels kwamba wanataka kuhakikisha dozi hizo zinasambazwa kwa kiwango walichokubaliana na AstraZeneca na kama walivyoahidi kwenye mkataba. Amesema mataifa yote 27 ya umoja huo yameunga mkono hatua hiyo.