Uingereza leo imeongeza vikwazo dhidi ya jeshi la Myanmar kufuatia hatua yake ya kuwakabili waandamanaji. 

Haya yamefanyika wakati ambapo kiongozi aliyepinduliwa Aung San Suu Kyi amefikishwa mahakamani. 

Uingereza ambayo ni mkoloni wa zamani wa Myanmar, imetangaza vikwazo dhidi ya Shirika la Kiuchumi la Myanmar MEC, shirika linaloendeshwa na jeshi la nchi hiyo ambalo Marekani tayari imeliharamisha. 

Uingereza pia itatoa dola laki saba kwa juhudi za Umoja wa Mataifa kunakili matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu nchini Myanmar. 

Vikwazo hivyo vimetangazwa wakati ambapo Suu Kyi amefikishwa mahakamani kwa njia ya video ambapo anakabiliwa na mashtaka kadhaa ya uhalifu ambayo huenda yakamzuia kuwania nafasi ya kisiasa katika siku zijazo.