Uingereza imelaani kile imesema kuwa ni uonevu wa jeshi la Myanmar baada ya balozi wa nchi hiyo mjini London kuondolewa katika mapinduzi ya kushangaza ya kidiplomasia baada ya kutoa wito wa kuwachiliwa huru kwa kiongozi wa kiraia Aung San Suu Kyi. 

Wanadiplomasia watiifu kwa watawala wa kijeshi Myanmar walichukua udhibiti wa ubalozi jana, na kumfungia nje balozi Kyaw Zwar Minn. 

Balozi huyo amesema afisa mkuu wa kijeshi amechukua usukani wa ubalozi huo katika aina fulani ya mapinduzi, ikiwa ni miezi miwili baada ya jeshi kukamata madaraka Myanmar. 

Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza Dominic Raab ametuma ujumbe wa kumuunga mkono balozi huyo, aliyelala usiku ndani ya gari lake nje ya ubalozi huo. 

Duru za Uingereza zimesema maafisa wa Myanmar walikuwa wameifahamisha serikali kuwa balozi huyo alikuwa ameondolewa katika wadhifa wake.