Uingereza imesema inapanga kufanya majaribio kadhaa ikiwemo kutoa hati maalum kwa watu waliopatiwa chanjo ya virusi vya corona ili kutathmini uwezekano wa kuwaruhusu kurejea tena kwenye maisha ya kawaida bila vizuizi. 

Mamlaka za nchi hiyo zimesema iwapo majaribio hayo yatafanikiwa, wale waliopatiwa chanjo ya covid-19 kikamilifu wataruhusiwa kujumuika tena ikiwa ni pamoja na kuhudhuria matamasha ya michezo, burudani na kumbi za starehe. 

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson anatarajiwa baadae leo kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu mipango ya kufanyika majaribio ya kutolewa kwa hati hizo. 

Hata hivyo wabunge kadhaa ikiwemo kutoka chama cha waziri mkuu Johnson cha Conservatives wanapainga mpango huo. Wakosoaji wengine wa mpango huo wamesema utoaji wa hati hizo utawatenga watu wa mataifa masikini ambao kwa sehemu kubwa bado hawajapatiwa chanjo dhidi ya virusi vya corona.