Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimeendelea kuwakaribisha wawekezaji kutoka nje na wawekezaji wazawa kuja kuwekeza Tanzania kwa sababu ya mazingira ya uwekezaji ni mazuri na yameboreshwa zaidi.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa Kanda ya Mashariki wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Bevin Ngenzi katika mwendelezo wa ziara za kutembelea wawekezaji ili kujione mafanikio pia changamoto wanazokabiliana nazo ili ziweze kufanyiwa kazi ambapo leo Aprili 22, 2021 aliambatana na ujumbe kutoka kwenye kituo hicho kutembelea uwekezaji uliofanywa na Mlimani Holdings Ltd wa kuwekeza katika mradi unaofahamika kama Mlimani City ambao wamewekeza katika vituo vya ununuzi vya maduka (shopping mall), kumbi za mikutano, nyumba za makazi mengi na majengo ya ofisi.

"Tunaipongeza serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya wawekezaji na tunawatia moyo na kuwakaribisha wawekezaji wengine, wawekezaji wazawa na wageni waweze kuja kuwekeza Tanzania, tuna mafanikio ya kibiashara, kuna utulivu wa kisiasa, kuna watu wema pia mahitaji mengine yanahitajika katika uwekeji yanapatikana kwa urahisi" Amesema Bw. Bevin Ngenzi, Meneja wa Kanda ya Mashariki wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Aidha, Bw. Bevin Ngenzi ameeleza kuwa Mradi huo ulifanywa kwa utashi wa Serikali ambao ulilenga kujenga maduka makubwa (shopping mall) na kumbi za mikutano za kimataifa pia ulikuwepo mpango wa kujenga hoteli ya nyota tatu na hayo yote yalilenga kutoa ajira na kuinua maisha ya watanzania lakini pia serikali iweze kukusanya mapato kutoka na biashara zinazoendelea kufanyika katika eneo hilo la Mlimani City.

Bw. Bevin Ngenzi ameendelea kwa kumpongeza mwekezaji wa mradi huo ambao unaendelea kufanya vizuri, mpaka sasa mradi umetoa ajira zaidi ya 2,000 pia biashara za watanzania zinaendelea kukua na kuimarika kupitia uwekezaji wa mradi huo huku akiwataka wawekezaji hao kuweka mpango wa kufanya uwekezaji huo katika mkoa wa Dodoma ambako ndiko yaliko makao makuu ya nchi lakini pia kuna ukuaji mkubwa wa biashara huku akiwahakikishia kuwa serikali itakuwa sambamba na kuhakikisha mipango yao inatimia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mlimani Holdings Ltd, Bw. Pastory Mrosso ameeleza kuwa tangu mradi ulipoanzishwa mwaka 2004, Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania imekuwa nyuma yao mafanikio makubwa ambayo yamepatikana ambapo Serikali ilikuwa sehemu yake ya kutekeleza na mwekezaji alikuwa na sehemu yake ya kutekeleza katika mradi huo.

Bw. Pastory Mrosso ameendelea kueleza kuwa serikali ina sehemu katika mradi huo ambapo hujipatia kodi kutoka kwa mwekezaji pamoja na wafanyabiashara walipo katika mradi huo, Pia mwekezaji analipa kodi kwa Chuo kikuu cha Dar es salaam ambapo mradi upo katika eneo lao huku akibainisha kuwa mpaka sasa zimetolewa ajira za moja kwa moja zaidi ya 2,000 na zipo ajira nyingi za muda kutokana na misimu ya biashara.