TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini TAKUKURU Mkoani Manyara, imefanikiwa kuokoa shilingi 32,400,434.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu, ameyasema hayo Mjini Babati, akizungumza na waandishi wa habari wakati akisoma taarifa ya robo tatu ya mwaka kuanzia mwezi Januari hadi mwezi Machi mwaka huu.

Makungu amesema zaidi ya kuokoa fedha hizo TAKUKURU imefanikiwa kurejesha mali mbalimbali ikiwemo magari manne, trekta moja, pikipiki moja na jembe la kukokotwa na ng’ombe.

Amesema katika kipindi hicho cha robo tatu ya mwaka, TAKUKURU ilifanya operesheni ya kiuchunguzi zilizolenga kurejesha fedha za Serikali zilizokuwa zichepushwe au kufanyiwa ubadhirifu kinyume na sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Amesema kupitia operesheni hiyo, kati ya fedha hizo shilingi 14,571,200.00 ni fedha za vyama vya ushirika yaani SACCOS na AMCOS, shilingi 10,504,000.00 zilirejeshwa kwa wanyonge ambao walikuwa wamedhulumiwa haki zao na shilingi 7,325,234.00 zilirejeshwa Serikalini.

Pia, amesema kwa kipindi hicho cha robo mwaka wamefanikiwa kupokea malalamiko 189 ambapo kati ya malalamiko hayo 122 yalihusiana na makosa ya rushwa na malalamiko 67 yalihusu makosa mengine ambayo walalamikaji walishauriwa na kuelekezwa katika ofisi husika kwa ajili ya utatuzi wa malalamiko yao.

“Jumla ya kesi tano mpya zilizofikishwa Mahakamani ikiwemo kesi namba CC.1/2021 ya Jamhuri dhidi ya Dunga Othman Omari ambaye uchunguzi umebaini ni mtumishi wa CCM anayeshtakiwa kwa kudaiwa kuwadhulumu wakulima watatu wa wilayani Hanang’ mwaka 2016 jumla ya shilingi milioni 58.4,” amesema.  

Amesema uchunguzi wao umebaini kuwa Dunga alijipatia fedha hizo kupitia kampuni ya Farm Green Imprements LTD kwa ahadi ya kuwaletea matrekta wananchi hao ila hakuwaletea wala kuwarejeshea fedha zao wananchi hao.

Amesema zaidi akaua kampuni ya Farm Green Imprements LTD aliyoitumia kujipatia fedha na kuanzisha kampuni nyingine ya PLANCON (T) LTD kitendo ambacho hutafsiriwa kuwa ni utakatishaji wa fedha zilizopatikana kwa njia isiyo halali.

“Nitumia nafasi hii kuwafahamisha watanzanina wote kwa ujumla kuwa ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imetoa usawa mbele ya sheria, aidha mamlaka zote za nchi zinapaswa kuwahudumia watu wote kwa msingi huo bila kujali utaifa wao, kabila mahali walipotoka, maoni yao kisiasa, rangi, dini, jinsi au hali yao ya maisha,” amesema Makungu.

Amesema ibara ya 107 A na 107 B za Katiba hiyo zimetoa mamlaka kwa mhimili wa Mahakama kuwa na kauli ya mwisho ya utoaji haki katika nchi ambayo kwa mujibu wa ibara hizo uhuru wa mahakama katika kutoa haki ya kila mmoja akiwemo Dunga umefafanuliwa.

“Kwa misingi hiyo ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakuna aliye juu ya sheria, hivyo sote tunapaswa kutii amri za kumtaka kufika bila shuruti Mahakamani ndiyo sababu utaratibu mwingine ambao hutumiwa na Mahakama kuwalazimisha washtakiwa kufika Mahakamani kwa kuwakamata kama ilivyofanyika kwenye kesi hii umetumika,” amesema.

Amesema katika kipindi cha Januarai hadi Machi, kesi nne zilitolewa hukumu, ambapo kesi tatu washtakiwa walipatikana na hatia na kupewa adhabu kwa mujibu wa sheria na kesi moja mtuhumiwa aliachiwa huru na kesi 39 zinaendelea mahakamani zikiwa katika hatua mbalimbali