Ndugu Wanahabari,

Kama mnavyofahamu Taifa letu bado lipo kwenye siku 21 za maombolezo baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt John Pombe Joseph Magufuli. Pamoja na tukio hilo kubwa la majonzi napenda kuwajulisha kuwa hali ya ulinzi na usalama nchini ni shwari ingawa kuna matukio machache ya kiuhalifu wa kijinai na ajali za usalama barabarani zilizotokea ambapo kwa pamoja yanaendelea kushughulikiwa na baadhi ya wahalifu waliohusika kutenda  matukio hayo wameshakamatwa.

Ndugu Wanahabari,
Kufuatana na kalenda ya kila mwaka, inapofikia wakati kama huu waumini wa dini ya kikristu husheherekea sikukuu ya Pasaka. Sikukuu hiyo hutanguliwa na mfungo na unapokaribia kumalizika juma la mwisho huwa na ibada mbalimbali ikiwa ni pamoja na  ibada ya Ijumaa Kuu, Jumamosi ibada ya usiku na Jumapili ambayo ndiyo sikukuu ya Pasaka tarehe 4.4.2021.  Siku hizi tatu waumini wa dini za kikristu hukusanyika kwa wingi katika nyumba za ibada kwa ajili ya sala.

Nipende kuwajulisha kuwa Jeshi la Polisi nchini limejipanga vizuri kuhakikisha kuwa waumini hao wanashiriki ibada hizo katika mazingira ya amani, utulivu na usalama na hata wananchi wengine kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

Wito wa Jeshi la Polisi Tanzania  ni kuomba ushirikiano kutoka katika kamati za ulinzi na usalama katika nyumba za ibada na sehemu zingine katika suala zima la kudumisha amani, ulinzi na usalama.

Ndugu Wanahabari,

Aidha, tunatoa rai na maelekezo kwa waendesha vyombo vya moto na watumiaji  wote wa barabara kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali ambazo kutokana na tafiti mbalimbali zilizowahi kufanyika zimeonyesha asilimia 75 ya ajali zinachangiwa  na uzembe wa binadamu.  Ajali zinaweza kuepukika kwa kiasi kikubwa kama kila mwananchi atafuata na kuzingatia sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kuepuka mwendo kasi,kutumia kilevi wakati wa kuendesha chombo cha moto,  kutokuzingatia alama za tahadhari za barabarani, kutokuvaa kofia ngumu (helmet) na kupakia mishikaki .

Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi wameshajipanga vizuri kuhakikisha hali ya usalama inaendelea kuimarika na kuwachukulia hatua kali wale wote watakaovunja sheria za usalama barabarani katika kipindi hiki kwani Makao Makuu ya Polisi imeshawapatia maelekezo na mikakati ambayo kila mmoja ataitekeleza kulingana na mazingira ya eneo lake na mipango ya kamati za usalama za himaya  husika.

Tuna imani  kama kila mwananchi atazingatia na kufuata sheria na kujiepusha na vishawishi vya kufanya vitendo vya kihalifu,  ibada za Pasaka zitamalizika  salama  tukizingatia kuwa bado tupo katika kipindi cha maombolezo na hatutegemei zile sherehe na shamrashamra tulizozizoea kipindi cha miaka ya nyuma kuwepo katika kipindi hiki.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Imetolewa na:
David A. Misime – SACP          
Msemaji wa Jeshi la Polisi
Makao Makuu ya Polisi
 Dodo­ma, Tanzania.