Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amewataka wabunge kuchangia Mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa kuishauri Serikali kama iendelee na mpango wake wa kununua ndege au isitishe hadi itakapoweka mambo sawa.

Ndugai amesema hayo bungeni mjini Dodoma leo Alhamisi Aprili 8, 2021 kabla kuchangia Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo (2021/22 hadi 2025/26) uliosomwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba.

Amesema Shirika la Ndege (ATCL) limepata hasara ya Sh60 bilioni, hivyo wabunge wanatakiwa kuishauri Serikali wakati wakichangia mpango huo kama iendelee na mpango wa kuongeza ununuzi wa ndege au wasitishe kwanza hadi watakapoweka mambo sawa.

Amewataka wabunge hao kushauri pia katika ununuzi wa mabehewa kwa ajili ya uendeshaji wa reli ya kisasa (SGR) kama ni vyema yakanunuliwa na Serikali au ununuzi ukafanywa na wabia wa sekta binafsi.

Amesema zipo nchi zinafanya uwekezaji wa miundombinu ya reli na suala la mabehewa linafanywa na wawekezaji binafsi.

Amewataka wabunge kutumia nafasi hiyo kuishauri Serikali na wasisubiri kukosoa wakati inapokosea.