Spika wa Bunge, Job Ndugai ameishauri serikali kuliangalia suala la mradi wa bandari ya Bagamoyo kama ni jambo jema iendelee nalo, huku akisema kuna wakati viongozi huwa hawashauriwi vizuri.

Akizungumza kabla ya kuahirisha shughuli za bunge jana mchana , Ndugai alikubaliana na ushauri wa Kamati ya Bunge ya Bajeti kuhusu mradi huo ambapo imeshauri serikali kuongeza kasi ya mazungumzo na wawekezaji ili bandari hiyo ianze kujengwa kwa kuwa manufaa yake ni makubwa kwa uchumi wa Taifa.

Spika Ndugai alisema “Nishukuru kamati ya bajeti kuona mradi wa bandari Bagamoyo, mimi nilisema wakati ule kwamba nimewahi kusafiri lakini sio safari ya mambo ya kibunge nilienda kwa ajili ya mambo ya bunge mtandao, nikakutana na ile bodi yenyewe kwa bahati mbaya.”

“Nilikuwa na wabunge wenzangu ilikuwa ni taarifa yenye ushawishi mkubwa, mkinipa nafasi Waziri wa Fedha nakumbuka zile hoja zote zile viongozi wetu hawawi briefed sawa sawa, kuna kuwa na watu wanawadanganya viongozi kabisa, kiongozi akisema mnanyamaza wote kwasababu ameshasema unaona hapa alikuwa mislead hapa alikuwa mislead,”

“Ni kampuni ya serikali wala sio ya binafsi na ina uchumi mkubwa mno nadhani ina bandari kadhaa kule China na duniani, tumebaki wachache ambao tunaijua hii project lakini tukiondoka hakuna kitakachokumbukwa kuhusu huu mradi utakuwa umekufa, kwasababu sisi ni watu wazima tunaelewa,” alisema.