Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Mei 8 mwaka huu linatarajia kuanza safari zake za moja kwa mona kutoka Tanzania kuelekea Guangzhou nchini China.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ametoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo yake na Balozi wa China hapa nchini Wang Ke.

Balozi Mulamula amesema kuwa safari hizo za moja kwa moja kutoka Tanzania kuelekea Guangzhou – China zitakuwa ni mara moja kila baada ya wiki mbili.
 
Kwa upande wake Balozi wa China nchini Wang Ke amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua yake ya kukutana na Jumuiya ya Wafanyabiashara kutoka China na kuongeza kuwa safari za ndege za moja kwa moja kutoka Tanzania hadi Guangzhou ni fursa ya kukuza biashara na uwekezaji katika ya Tanzania na China.
 
Kwa nyakati tofauti Waziri huyo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika pia amekutana na kufanya mazungumzo na Mabalozi kutoka Ujerumani, Ubelgiji na Israel wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni kuimarisha ushirikiano, uchumi na biashara.
 
Balozi wa Israel nchini Oded Joseph amemueleza Balozi Mulamula kuwa nchi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali hususani kwenye kukuza ujuzi wa kilimo chenye tija kwa vijana.

Kwa sasa, Israel inawapokea vijana kutoka Tanzania waliohitimu katika vyuo vya kilimo kwa lengo la kujifunza kwa vitendo nchini humo.