Afisa mwandamizi wa Shirika la Afya Duniani, WHO amesema watu waliokufa kwa COVID-19 barani Ulaya wamepindukia milioni moja. 

Mkurugenzi wa WHO barani Ulaya, Dokta Hans Kluge amesema hali bado ni mbaya, huku takriban visa vipya milioni 1.6 vya virusi vya corona vikirekodiwa katika bara hilo kila wiki. 

Akielezea wasiwasi wa hivi karibuni kuhusu chanjo, Kluge pia amesema hatari ya watu kupatwa na matatizo ya damu kuganda ni makubwa zaidi kwa watu wenye virusi hivyo kuliko watu wanaopewa chanjo ya AstraZeneca. 

Wakati huo huo, Waziri wa Afya wa Ujerumani, Jens Spahn ameyaomba majimbo yote ya nchi yake kuweka mara moja hatua zaidi za kuzuia kuenea kwa virusi vya corona, kuliko kusubiri hadi wakati wa dharura.