Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, ametembelea na kukagua barabara ya Malinyi mkoani Morogoro iliyoharibika kutokana na maji ya Mto Furuwa kufurika na kupita juu ya barabara na hivyo kukata mawasiliano kati ya kijiji cha Misegese na Malinyi mjini

Mhandisi Kasekenya amefika wilayani Malinyi kufuatia kero ya maji ya Mto Furua inayotokana na kupungua kwa kina cha mto huo na kusababisha maji kupita juu ya barabara ya Malinyi katika eneo la Mwembeni kijiji cha Misegese na hivyo kusababisha barabara hiyo kutopitika na hivyo wananchi wa kijiji hicho kukosa huduma za kijamii zinazopatikana upande wa pili ambako ni Malinyi mjini.

“Nawashukuru sana wananchi wa Malinyi kwa mliojumuika nasi hapa kuelezea changamoto za barabara hii zinazotokana na kufurika kwa mto Furua, tayari nimeshamtuma Mkurugenzi wa Matengenezo ya Barabara kufika hapa na kushirikiana na wataalamu Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Morogoro, na kuhakikisha kuwa taratibu za kitaalamu zinafuatwa katika kutengeneza barabara hii, baada ya uharibifu uliotokea ili iweze kupitika katika majira yote ya mwaka”. amesema Mhandisi Kasekenya

Nae Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Mathayo Masele alimshukuru Naibu Waziri Kasekenya kwa kufika wilayani hapo na kumuambia kuwa ofisi yake tayari imechukua hatua mbalimbali ikiwemo ya kujenga tuta na kupanda miti na majani ili kuzuia maji hayo kukatiza barabarani, lakini bado kero imekuwa kubwa kutokana na kupungua kwa kina cha mto Furua.

“Nawashukuru sana TANROADS mkoa wa Morogoro kwa ushirikiano mzuri tangu tatizo hili lilipojitokeza, na sisi kama Serikali ya Wilaya tunaahidi kuweka ulinzi wa kutosha mara baada ya matengenezo ya barabara hii kukamilika kwa kuhakikisha kuwa shughuli za kilimo hazifanyiki katika maeneo ya hifadhi ya barabara pamoja na maeneo ya vyanzo vya maji ili kuzuia uharibifu wa barabara hii”.  Alisisitiza Masele

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Malinyi Mhe. Antepas Mgungusi alisema kuwa wananchi wa kijiji cha Misegegese wanapata tabu sana pindi barabara hii inaposhindwa kupitika kutokana na maji ya mto Furua kupita juu ya barabara kwa sababu huduma za kijamii zinapatikana upande wa pili wa mto ambako ni Malinyi mjini.

“Tunawaomba TANROADS kama itawezekana mchonge njia ya maji kwenye mto huu pamoja na kuongeza kina chake ili maji yapate njia ya kupita na yasifurike tena na sisi tutakuwa macho kuwafichua wale wote watakaofanya shughuli za kilimo ndani ya meta 60 za hifadhi ya barabara” Amefafanua Mgungusi.

Aidha meneja wa TANROADS mkoa wa Morogoro alimuambia Naibu Waziri Kasekenya kuwa ofisi yake imejipanga kuikarabati barabara hiyo kwa kuongeza makaravati sehemu zitakazohitajika kufanya hivyo pamoja na kuinyanyua barabara hiyo ili maji ya mto huo yasipite juu ya barabara, na kwamba utekelezaji wake unaanza mara moja.

Naibu Waziri Kasekenya alikuwa mkoani Morogoro kwa zira ya kikazi ya siku mbili, ili kukagua miundombinu ya barabara iliyoharibika kutokana na mafuriko yatokanayo na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.