Rais wa Urusi Vladmir Putin na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wameelezea wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mivutano mashariki mwa Ukraine. 

Mazungumzo yao ya njia ya simu yamekuja wakati makabiliano kati ya wanaharakati wanaopigania kujitenga wakiungwa mkono na Urusi na wanajeshi wa Ukraine yakiongezeka katika wiki za karibuni, nalo jeshi la Urusi likijikusanya katika mpaka wa nchi hizo hali iliyoongeza hofu ya mgogoro huo kuwa mbaya hata zaidi. 

Mapema leo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alitembelea uwanja wa mapambano katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo la Donbass. Katika siku za karibuni Zelensky alitoa mwito kwa washirika wa nchi yake wa magharibi kumpa msaada katika mzozo huo. 

Merkel na Putin pia walijadili suala la kiongozi wa upinzani Urusi Alexei Navalny ambaye wiki iliyopita alifanya mgomo wa kula gerezani akidai kupewa matibabu bora ya maumivu ya mgongo na tatizo la kufa ganzi kwenye miguu yake. Aidha walijadili mzozo wa Syria na mgogoro wa kisiasa Libya.