Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa

Akizungumza leo Jumanne Aprili 6, 2021, Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa kuwaapisha makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu amesema wizara ihakikishe vyombo vya habari vinafuata sheria na miongozo iliyoweka.

“Nasikia kuna vyombo vya habari mlivifungia, vifungulieni na vifuate sheria tusiwape mdomo kwamba tunaminya uhuru wa kuzungumza. Tusifungie kibabe, wafungulieni na kuhakikisha wanafuata kanuni na miongozo ya Serikali.

“Watakapofanya makosa adhabu zitolewe kulingana na sheria inavyoelekeza, viacheni vifanye kazi yao isionekane wanazuiwa kuongea,” amesema Samia.

Rais pia amesisitiza wizara hiyo ambayo inahusika pia na michezo, sanaa na utamaduni kusimamia haki za wasanii na wanamichezo kuhakikisha kundi hilo wananufaika na kazi zao.