Rais  Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inaangalia namna ya kulilea Shirika la Ndege nchini (ATCL) kimkakati ili lijiendeshe kwa ufanisi.

Amesema hilo litafanyika kwa kuangalia uwezekano wa kutoa nafuu wa madeni na baadhi ya kodi na tozo kama inavyofanyika katika nchi nyingine ili liweze kukua na kuweka hesabu zake sawa.

Ameeleza hayo  Alhamisi Aprili 22, 2021 wakati akilihutubia Bunge mjini Dodoma.

“Shirika letu sasa hivi linasomeka kwamba ni shirika la deficit, halina thamani lakini ni kwa sababu ya kurithi madeni makubwa ya nyuma, hivyo kama Serikali tunakwenda kulitua mzigo wa madeni makubwa.”

“Pia tutalipa unafuu wa kodi na tozo ili liweze kukua, sote tunafahamu kuwa biashara ya ndege ni ngumu, tutajitahidi kusoma mwenendo wa biashara hii ulimwenguni na kuepuka mambo yote yasiyo na tija kwa Taifa letu,” amesema.

Amesema Serikali haitakubali kuona shirika linaendelea kupata hasara baada ya uwekezaji mkubwa na kwamba  uwekezaji pia utafanyika kupata rasilimali watu wenye uwezo na weledi wa kuendesha shirika kibiashara.

“Hii ina maana tunakwenda kulifanyia uchambuzi wa kina na kuhakikisha tutakaowaamini kuliendesha shirika ni watu wenye weledi na watakaoweza kuliendesha kibiashara,” amesema Samia.