Rais Samia Suluhu Hassan atahutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 22, 2021.

Spika wa Bunge, Job Ndugai amelitangazia Bunge leo Jumatatu Aprili 19, 2021 kuwa Rais Samia atalihutubia Bunge Alhamisi ya wiki hii kuanzia saa 10 jioni.

Hivyo, Spika Ndugai amewaagiza wabunge wote walioko nje ya Jiji la Dodoma kurudi na wale wanaotaka kuondoka wazingatie kuwapo kwa shughuli hiyo kwanza.

Rais Samia atalihutubia Bunge kwa mara ya kwanza tangu alipoapishwa kuwa Rais Machi 19, 2021 baada ya kifo cha Rais wa tano, John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021.

Rais Samia atatoa hotuba hiyo wakati chama chake (CCM) kiko kwenye maandalizi ya mwisho kuelekea Mkutano Mkuu wa dharura utakaofanyika Jijini Dodoma Aprili 30.

Kwa mujibu wa Ndugai, baada ya hotuba hiyo, Rais Samia atashiriki futari aliyoiandaa kwa wabunge na wageni wengine katika viwanja vya Bunge.