RAIS Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewataka Watazania waendeleze utamaduni wao uliodumu kwa muda mrefu wa kushikamana, kupendana na kushirikiana ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa ya amani na utulivu.
 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameyasema hayo jana (Ijumaa, Aprili 2, 2021) baada ya sala ya Ijumaa katika msikiti wa Gaddaf jijini Dodoma. Waziri Mkuu alikuwa akiwasilisha salamu za Rais Mheshimiwa Samia kwa Watanzania.
 
Amesema Mheshimiwa Rais Samia anamatumaini makubwa na Watanzania wote hivyo amewataka waendelee kuwa watulivu na washiriki katika shughuli mbalimbali kwa ajili ya kuboresha maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
 
“Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anamatumaini makubwa kwa Watanzania wote, tuendelee kuliombea Taifa letu na kila mmoja ashiriki katika shughuli za maendeleo na hatua tunayotarajia itafikishwa na sisi wenyewe na tukizingatia haya tutafanikiwa sana.”
 
“Serikali inaendelea na kazi na hivi karibuni tutaanza ujenzi wa ofisi mpya za kudumu za Wizara kwa sababu zilizopo zilikuwa za muda tu. Mkakati wa muendelezo wa kuifanya Dodoma kuwa makao makuu unaendelea.”
 
Amesema Serikali imejipanga ipasavyo kuhakikisha wananchi wanaendelea kuhudumiwa na kutumikiwa huko huko walipo. “ Serikali ipo imara na imejipanga vizuri kuwahudumia na hakuna kitakachoharibika Watanzania waendelee kuwa na imani na Serikali yao, yote yaliyopangwa yataendelezwa.”
 
Akizungumzia kuhusu miradi mkubwa ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa nchini, Waziri Mkuu amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan  imejipanga vizuri kuhakikisha miradi yote inaendelea kutekelezwa kama ilivyopangwa,
 
Hivyo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasisitiza Watanzania wamuombee kwa Mwenyezi Mungu Rais pamoja na wasaidizi wake wote ili waendelee kutimiza majukumu yao ya kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo yanatimia.
 
“Tumeanza vizuri, tutaendelea vizuri na tutamaliza vizuri, wananchi tuendelee kumuombea rais wetu ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu aendeee kuwa na afya njema ili atekeleze malengo ya kuwatumikia Watanzania na hakuna kitakachoharibika.”
 
Kadhalika Waziri Mkuu ameedelea kuwasisitiza wazazi na walezi nchini kuhakikisha wanawajengea watoto wao msingi wa kufanya ibada kwa kuongozana nao kwenye nyumba za ibada kwa kuwa dini zinanafasi kubwa ya kuwakuza katika maadili mema.