Rais  wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema viongozi wa kitaifa wakikutana na mabango katika ziara zao, atawaondoa kazini mkurugenzi wa halmashauri na wakuu wa wilaya husika.

Aidha, Rais Samia amewaagiza Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu pamoja na Wakuu wa Taasisi mbalimbali aliowaapisha hii leo kufanya kazi kwa kutenda haki na sio kuwanyanyasa wanaowaongoza.

Rais Samia ametoa maagizo hayo Ikulu jijini Dar es salaam alipokuwa akiwaapisha viongozi hao na kuongeza kuwa katika uongozi wake hatapenda kuona viongozi anaowateua wanawanyanyasa wanaowaongoza na jambo hilo likitokea ataamua vinginevyo.

Kuhusu kero mbalimbali za Wananchi, Rais Samia Suluhu Hassan ametaka kushughulikiwa kwa kero hizo kwa uharaka na si kusubiri viongozi wakuu akiwemo yeye mwenyewe, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu.

Amesema katika ziara zake akiona bango la malalamiko ya Wananchi na utatuzi wa jambo hilo liko ndani ya uwezo wa viongozi wa ngazi ya chini, Mkuu wa wilaya ama Mkurugenzi wa  halmashauri ataondolewa katika wadhifa wake.

 “Tumezoea tunapokwenda kwenye ziara mikoani  na wilayani tunapokelewa na mabango ya wananchi wakilalamika kero mbalimbali, mabango yale mengine wala siyo mambo au masuala ya kushughulikwa katika ngazi za juu ni masuala ya kushughulikwa huko chini.

“Kwa hiyo naomba tunapokuja huko mimi na makamu wa rais, waziri mkuu tukikuta bango basi ziwe inshu ya kitaifa lakini siyo mambo ya kushughulikiwa kule chini, nataka niseme  bango moja aidha mkurugenzi au mkuu wa wilaya amekwenda na hii  haina maana mkazuie watu kuandika kero zao,” amesema.