Rais Samia Suluhu Hassan leo amepokea ujumbe maalum kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya uliowasilishwa na Waziri wa Michezo, Utamaduni na Urithi wa nchi hiyo Balozi Amina Mohamed.

Pamoja na kupokea ujumbe huo Ikulu jijini Dar es salaam, Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mazungumzo na Balozi Amina yaliyohusu dhamira ya Tanzania na Kenya kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano katika nyanja mbalimbali.

Rais Samia Suluhu Hassan amemhakikishia Rais Kenyatta kuwa Serikali anayoiongoza ipo tayari kuendeleza mambo mazuri yote yaliyokuwa yakifanywa na mtangulizi wake Hayati Dkt. John Magufuli na kutatua changamoto kati ya Tanzania na Kenya kwa kuwa nchi hizo ni ndugu, majirani na marafiki wa kihistoria.

Amewataka Mawaziri na Wataalam wa Tanzania na Kenya wanaounda Kamati ya Ushirikiano wa Pamoja ambao hawajakutana tangu mwaka 2016 kukutana mara moja ili kufanyia kazi masuala mbalimbali ya kuimarisha uhusiano.

Rais Kenyatta amemwalika Rais Samia Suluhu Hassan kufanya ziara rasmi nchini Kenya ili kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano.

Amemhakikishia Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Kenya ipo tayari wakati wote kushirikiana na Tanzania kwa kuendeleza na kukuza zaidi ushirikiano kati ya nchi hizo.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Amina aliongozana na Balozi wa Kenya hapa nchini Dan Kazungu.