Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali, ambapo amemteua Dkt. Richard Masika kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT).

 Dkt. Masika anachukua nafasi ya Marehemu Profesa Apollinary Peleka.

Profesa Joseph Msambichaka ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) kuchukua nafasi ya Profesa Manase Salema.

Rais Samia Suluhu Hassan pia  amemteua Dkt. Revocatus Mushumbusi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Ladislaus Nshubemuki ambaye amestaafu.

Profesa John Kandoro yeye ameteuliwa kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) baada ya kumaliza muda wa kipindi cha kwanza.

Uteuzi mwingine ni wa Dkt. Mboni Ruzegea ambaye anakuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Ali Mcharazo ambaye amestaafu.

Kiongozi mwingine aliyeteuliwa na Rais Samia.Suluhu Hassan ni Profesa Esther Lugwisha ambaye anaendelea kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali baada ya kumaliza muda wa kipindi cha kwanza.

Kepteni Ernest Bupamba ameteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) baada ya kumaliza kipindi cha kwanza.

Profesa Makenya Maboko ameteuliwa kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) baada ya kumaliza muda wa kipindi cha kwanza.