RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametengua uteuzi wa Makamanda watatu wa Idara Maalum za SMZ kufuatia kuwepo kwa wafanyakazi hewa na kusababisha upotevu wa fedha nyingi za Serikali.


Waliotenguliwa ni Kamanda wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar Ali Abdallah Ali, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Kanali Ali Mtumweni Hamad pamoja na Mkuu wa Kikosi Maalum Cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM) Comodore Hassan Mussa Mzee.


Akitoa taarifa kwa wananchi kupitia vyombo vya Habari Ikulu Jijini Zanzibar,Dk. Mwinyi alisema kuwa kufuatia taarifa za uwepo wa wafanyakazi hewa katika Idara Maalum za SMZ, aliumda Kamati ya Uchunguzi kwa kufanya uhakiki wa idadi ya wafanyakazi pamoja na viwango vya mishahara vinavyotolewa kwa vikosi vyote.


Alisema kuwa ripoti ya Kamati ya Uhakiki iliyomfikia ilieleza kwamba kulikuwa na wafanyakazi 381 waliokuwa wakilipwa mishahara bila ya kuwa katika utaratibu unaotakiwa ikiwa na maana kwamba walikuwa watumishi hewa.


Alisema kwamba fedha zilikuwa zikipokelewa na kutumika katika kipindi chote hicho ambapo walikuwa katika vikosi hivyo na kueleza kwamba lililothibitika ni kwamba wakati Kamati imeanza kazi zake baadhi ya vikosi kikiwemo JKU walianza kutengeneza utaratibu wa kurasimisha uwepo wa wafanyakazi hao hewa.


Alisema kwamba waliwahi kukamatwa baadhi ya Maafisa katika nyumba ya mtu binafsi wakiwa wamewafisha sare za Jeshi vijana na kuwapiga picha ili kuthibitisha kwamba wamo katika ajira rasmi.


Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba  imebainika kuwa fedha zilizotumika kwa upotevu ni kiasi cha TZS  bilioni 2,235,725,000.00 kutokana na fedha zilizokuwa zikitumika kwa wafanyakazi hewa.


Vile vile, Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba Kamati ilikwenda kuhakiki ulipaji wa posho katika vikosi hivyo ambapo ilibaini wastani wa upotevu wa fedha zilizokuwa zikilipwa kwa ajili ya posho kwa mwezi wa Disemba ni jumla ya TZS milioni 304,135,939.00 sawa na wastani wa TZS bilioni 1,824,815,634.00 kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Julai hadi Disemba.


Alisema kwamba Kamati haikuishia hapo na iliendelea kubaini kwamba kuna watumishi ambao walikuwa wameshastaafu lakini bado walikuwa wakiendelea kupokea mishahara ambapo kuliwa na wastaafu 12 wa Idara Maalum za SMZ waliokuwa wakiendelea kulipwa mishahara baada ya kustaafu ambapo ni kinyume na utaratibu.


Alieleza kwamba hali hiyo imesababishwa na wahasibu wakuu wa Idara Maalum za SMZ kwa uzembe ama kwa kukusudia ambapo kwa misingi hiyo Serikali imeingia hasara ya jumla ya TZS milioni 44,610,280.00.


Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa wastaafu wawili waliitwa na Kamati na kuhojiwa na baadae walikubali kurejesha fedha jumla ya TZS milioni 10,766,560.00 fedha ambazo ziliingizwa katika mfuko mkuu wa Serikali.


Alisema kwamba hayo yote yanabainisha kuwa ni kweli kulikuwa kuna watumishi wameshastaafu na bado walikuwa wakilipwa mishahara kinyume na utaratibu.


Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba mtumishi anapofukuzwa kazi hutakiwa kuwekewa kizuizi cha mishahara mara tu anapofukuzwa kazi hata hivyo, Kamati imegundua kwamba wahasibu wakuu wa  vikosi  pamoja na waingizaji wa taarifa za mishahara huchelewesha mchakato huo kwa makusudi ili fedha hizo zitumike katika matumizi yao binafsi.


Hivyo, Kamati imegundua kwamba wahasibu huwatengenezea madeni watumishi  waliokuwa wamefukuzwa kazi na fedha hizo hukatwa na kupelekwa kwenye duka la kikosi na hatimae fedha hizo huingia mifukoni mwa wahasibu hao ambapo jumla ya fedha zilizopotea kwa aina hiyo ni kiasi cha TZS 117,724,000.00.


Aidha, alisema kuwa Kamati imebaini kwamba kuna ukataji wa Posho ya chakula kwa askari Kapera kinyume na utaratibu kwani kwa kawaida askari anapojiriwa hukaa Kambini kwa kipindi cha miaka miwili na kukatwa posho ya chakula ya kiasi cha TZS 70,000 kwa kila askari kwa kila mwezi fedha ambazo ni kwa ajili ya kujikimu.


Alisema kwamba kwa upande wa JKU Kamati imebaini kwamba jumla ya askari 771 walikatwa fedha za posho ya chakula bila ya kukaa Kambini na fedha zao kuingia mifukoni mwa watu wachache kiasi cha TZS 539,700,000.00 kwa kipindi cha miezi kumi kuanzia mwezi wa Machi 2020 hadi Disemba 2020.


Pia, Kamati hiyo imebaini kwamba Maafisa na askari wananyimwa fursa ya kupata vielelezo vya taarifa za mishara yao ikiwemo ‘Payslip’ zao  hiyo imepelekea kwa baadhi ya askari hao kukatwa mishahara yao kinyume na utaratibu na kutokujua malengo ya makato hayo.


Alisema kuwa Kamati hiyo pia, imegundua kuwa kuna baadhi ya Askari waliokuwa wakitiliwa posho na kukatwa kwa kuingizwa kwenye maduka ya vikosi hali ambayo iliibua malalamiko mengi kwa askari na kuwakosesha morali ya kufanya kazi.


Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa takriban askari wote walikiri kuwa kwa mara ya kwanza  baada ya kuanza uhakiki huo ndipo wamepewa ‘Payslip’ zao pamoja na kujua stahiki zao.


Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa pamoja na Kamati kufanya kazi nyingi na kugundua udhaifu sehemu nyingi sana inatosha kwa hayo yaliobainika kuweza kuchukua hatua za kisheria ambapo aliagiza wahasibu na waingizaji wa data wachukuliwe hatua za kisheria na tayari wameshasimamishwa kazi na utaratibu wa kuchukuliwa hatua za kisheria unaendelea.