Kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis, amewahimiza waumini kutopoteza tumaini kufuatia janga la muda mrefu la virusi vya corona.

Mamilioni ya waumini wa dini ya Kikristo duniani wanashehekea leo sikukuu ya Pasaka chini ya vizuizi vikali vya kukabiliana na virusi vya corona ambavyo maambukizi yake bado yanaongezeka kwenye mataifa mengi ulimwenguni.

”Katika saa ya giza wakati binadamu anapambana na janga la Corona pamoja na magonjwa mengine, Wakristo wanapaswa kuzingatia ujumbe wa malaika wakati wa Pasaka wa kutoogopa”.

Papa Francis mwenye umri wa miaka 84 ameyasema hayo usiku wa Jumamosi Takatifu katika kanisa la Mtakatifu Petero mjini Roma Italia, wakati wa mkesha wa Pasaka.

Kwenye ujumbe wake mmoja wa Pasaka, Papa Francis amesema inawezekana kila wakati kuanza upya. Hata kwenye historia ya vurugu ya mwanadamu, Mungu ameumba kitu kipya.

”Kutoka kwenye vipande vya mioyo yetu, Mungu anaweza kuumba kazi ya sanaa; kutokana na mabaki ya ubinadamu, Mungu anaweza kutengeneza historia mpya,” amesema Papa na kuongeza kuwa ”katika miezi hii ya giza la janga… msikilize Yesu Aliyefufuka. Anatualika tuanze upya na tusipoteze tumaini”.
 
DW