Wakristu kote ulimwenguni jana wameadhimisha siku ya Ijumaa Kuu huku kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis akiiadhimisha siku hiyo akiwa chini ya vikwazo vikali kufuatia janga la virusi vya corona. 

Ilipofika saa 12.00 za jioni Papa Francis aliadhimisha kumbukumbu ya kuteswa kwa Yesu Kristu katika ibada ilikayofanyika kwenye Kanisa la Mtakatifu Petro wa Basilica. 

Kulingana na Vatican ni waumini wachache tu waliruhusiwa kuhudhuria ibada za Papa katika sikukuu za Pasaka kwa sababu ya hatua za kuzuwia kusambaa kwa virusi vya corona. 

Kama ilivyokuwa mwaka jana mwaka huu pia hakukuwa na ibada ya Njia ya Msalaba ambayo kwa kawaida hufanyika katika eneo la Colosseum katikati ya jiji la Rome. 

Na badala yake kulifanyika ibada ndogo za Njia ya Msalaba katika bustani ya Mtakatifu Petro mbele ya Kanisa la Basilica.