Na Mwandishi wetu, Hanang'
MRATIBU chanjo wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang' Mkoani Manyara, Mkojera Philemon Mkojera amenusurika kwenda jela miezi 12 baada ya Mahakama ya Hakimu mkazi wa Wilaya hiyo, kumhukumu kulipa faini ya sh950,000 kwa kosa la kughushi.

Hakimu Mkazi wa mahakama ya Wilaya ya Hanang' Samwel Mushumbusi ametoa hukumu hiyo kwenye mahakama hiyo ya kulipa faini hiyo ya shilingi 950,000 kwa makosa 19 ya rushwa na kufanikiwa kuepuka kifungo cha miezi 12.

Hakimu Mushumbusi ametoa hukumu hiyo kwa makosa ya kughushi kinyume na kifungu cha 333,3335 (a) 337, vya sheria ya kanuni ya adhabu na ubadhirifu kinyume na kifungu cha 28 (1) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007.

Mratibu huyo wa chanjo wa halmashauri ya wilaya ya Hanang' Mkojera, amelipa faini ya shilingi 50,000 kwa kila kosa kati ya makosa 19 aliyoshtakiwa kwa kughushi.

Hata hivyo, Mkojera anatarajiwa kufikishwa tena mahakamani kwa makosa mengine ya matumizi ya nyaraka ya kumdanganya mwajiri wake kinyume na kifungu cha 22, ubadhirifu kinyume na kifungu cha 28 (1) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 1/2007 pamoja na uhujumu uchumi tofauti na kesi aliyohukumiwa Machi 31.

Awali, Mkojera alifikishwa mahakamani hapo na mawakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Martin Makani na Eveline Onditi kwa makosa 19 yakiwemo ya kughushi na ubadhirifu wa fedha.

Mkojera alifanya makosa hayo Octoba 2014 katika maeneo mbalimbali Wilayani Hanang' kwa kughushi majina na sahihi za watu 18 kuwa aliwalipa posho watu 10 shilingi 240,000  kila mmoja na watu nane shilingi elfu 70 wakati wa chanjo ya surua na rubela.

Hata hivyo, Mkuu wa TAKUKURU mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu ameelekeza endapo Mkojera hajaondolewa katika utumishi wa umma basi halmashauri ya Hanang' ianze mchakato wa kukuondoa kwenye utumishi wa umma kwa mujibu wa kanuni ya utumishi wa umma za mwaka 2003.

Makungu amesema Mamlaka hiyo ya nidhani iangalie kwamba kwa mujibu wa kanuni za kudumu za utumishi wa umma za 2009 kanuni F39 (3) mtumishi wa umma akipatikana na hatia ya makosa ya jinai yatokanayo na rushwa na ubadhirifu wa fedha au mali ya umma, kama ilivyo kwa Mkojera hupoteza stahili zake zote katika utumishi wa umma.

"Ni rai yetu kwa watumishi wa umma kujiepusha na vitendo vya rushwa na ubadhirifu ili kuepuka kupoteza haki zao kwenye utumishi wa umma kama Mkojera atakavyopoteza kutokana na ubadhirifu wa shilingi 2660,000 alioufanya," amesema Makungu.