Nyambizi ya jeshi la Indonesia iliyopotea mapema wiki hii imepatikana chini ya bahari ikiwa imekatika vipande vitatu na wafanyakazi wote 53 waliokuwemo wamefariki dunia. 

Jeshi la Indonesia limetoa taarifa hiyo jana Jumapili likisema limeyapata mabaki ya nyambizi hiyo umbali wa futi 2,600 chini ya bahari baada ya kutuma chombo kingine kidogo kilichotolewa na Singapore. 

Mkuu wa jeshi la Indonesia Hadi Tjahjanto, amesema mabaki mengine ya chombo hicho ikiwemo nanga na mavazi ya usalama yaliyovaliwa na wafanyakazi waliokuwemo pia yamepatikana. 

Taarifa hizo za simanzi zimekuja kiasi siku nne tangu nyambizi hiyo ilipotoweka Jumatano iliyopita wakati ikifanya mazoezi ya kufyetua makombora kutokea majini nje kidogo ya pwani ya kisiwa cha Bali.