Kiongozi wa upinzani nchini Urusi aliyeko kifungoni Alexei Navalny amehudhuria kikao cha mahakama kwa njia ya video. 

Akiwa amenyoa nywele zake, Navalny ameonekana akiwa mdhaifu baada ya kumaliza mgomo wake wa kula. 

Kikao hicho cha mahakama kinahusiana na jaribio lake la kubatilisha hukumu na faini aliyopewa mwezi Februari kwa madai ya kumchafulia jina shujaa mmoja wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. 

Kama iliyotarajiwa, mahakama imeunga mkono hukumu hiyo, kumaanisha kuwa Navalny lazima alipe faini hizo za kiasi cha dola 11,400, ambacho ni karibu mara mbili ya wastani wa mshahara wa kila mwaka nchini Urusi. 

Mawakili wake wametangaza kuwa wataipeleka kesi hiyo katika Mhakaama ya Ulaya ya Haki za Binaadamu. 

Wakati huo huo, mwanachama mwandamizi wa mtandao wa Navalny amesema timu za kikanda za mwanasiasa huyo zitasitisha kazi zao kutokana hatua ya karibuni ya mahakama.