Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye, amesema kwa mujibu chama hicho tawala, kukosoa na kujikosoa ni silaha ya mapinduzi na kujiimarisha na siyo dalili ya udhaifu.

Nape amesema hayo wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya waziri mkuu na taasisi zake kwa mwaka 2021/22.

Amesema Rais wa awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan ameanza vizuri na kutaka wananchi kumpa ushirikiano,

“Tusigombane bila sababu, Tanzania ni yetu sote tumsaidie mama naye aandike kitabu chake tusimshike mkono kumwandikia kitabu tumwache aandike kitabu chake na ndugu zangu legacy (alama) haitetewi inajitetea yenyewe.

“Hasa ile inayofanywa na mtu kama Magufuli itajitetea na kujisimamia miaka labda kama mtu ana mashaka na legacy yake lakini kama hamna mashaka na legacy yake itasikilizwa, itaongewa sisi watoto wajukuu na vitukuu kwa sababu haya waliyoyafanya watayakuta,” amesema.

“Mimi nimekuwa kiongozi katika chama, nimesimamia idara ya maktaba na nyaraka duniani hakuna chama bora kilicho document vya kutosha CCM ni karibia namba moja kwa kila kitu,” amesema.

Amesema kwenye nyaraka zao wamesema kukosoa na kujikosoa ni silaha ya mapinduzi na kujiimarisha na sio dalili ya udhaifu.