Mazishi ya mume wa Malkia Elizabeth II wa Uingereza, Mwanamfalme Philip, yatafanyika wiki ijayo. 

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa kasri la Buckingham, mazishi hayo yataendeshwa kwa taratibu tofauti kutokana na vizuizi vya kupambana na janga la virusi vya corona. 

Shughuli ya mazishi itarushwa moja kwa moja kupitia televisheni, Aprili 17, saa nane mchana, katika kanisa la Mtakatifu George, magharibi mwa London. 

Mjukuu wake, Harry, ambaye kwa siku za karibuni, yeye na mkewe Meghan wamekuwa na mzozo na familia ya kifalme, atahudhuria mazishi hayo, ambayo yatawashirikisha watu 30 tu wa karibu. 

Bendera zitapepea nusu mlingoti kwenye majengo ya serikali hadi baada ya mazishi. Mwanamfalme Phillip, aliyekuwa mume wa Malkia Elizabeth kwa kipindi cha miaka 73, alikufa juzi Ijumaa akiwa na umri wa miaka 99.