Jeshi la Polisi mkoani Kagera  linamtafuta mtu aliyehusika na mauaji ya mtoto mwenye umri wa miaka kumi, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Kahororo manispaa ya Bukoba.

Mwanafunzi huyo awali alibakwa kwa kulawitiwa na kisha kupigwa kitu kizito kichwani.
 

Kamanda wa polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi  alisema mtoto huyo alitoweka nyumbani kwao Aprili 5 baada ya kutumwa na mama yake dukani kwenda kununua sabuni.

“Baada ya kusubiri kwa muda mrefu bila mtoto kurejea nyumbani, mama huyo aliamua kwenda kumuulizia dukani ambapo muuzaji alimweleza kuwa hakuwa amefika dukani hapo,” alisema Malimi

“Akishirikiana na majirani mama huyo alimtafuta mtoto wake bila mafanikio hadi siku iliyofuata mwili wa marehemu upokutwa kwenye vichaka kandokando mwa Ziwa Victoria eneo la Rwazi,” alisema Malimi

Alisema uchunguzi wa kitabibu ulibaini kuwa mtoto huyo alibakwa na kulawitiwa kutokana na alama zilizokutwa sehemu zake za siri, huku akiwa na jeraha kubwa kichwani.

Kamanda Malimi aliwaomba watu mwenye taarifa zitakazosaidia kuwabaini na kuwatia mbaroni wahusika, kujitokeza kwa siri kuzitoa kwa polisi au viongozi wa Serikali za Mitaa.