Jeshi la Polisi mkoa wa kipolisi Kinondoni linamshikilia mtu mmoja kufuatia kifo cha aliyekuwa mtangazaji wa ITV, Blandina Sembu.

Usiku wa kuamkia Machi 27, 2021 mwili wa Blandina ulikutwa pembezoni mwa barabara mita chache kutoka baa ya Mary Land iliyopo eneo la Mwenge, njiapanda ya kuelekea ITV jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na moja wa chombo cha habari, Kamanda wa polisi wa mkoa huo, Ramadhani Kingai alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na katika hatua za awali wanamshikilia mtu mmoja ambaye hakumtaja jina lake .

Kingai alisema jina na mtuhumiwa huyo linahifadhiwa kutokana na sababu za kiupelelezi.

Kwa mujibu taarifa iliyotolewa na Kamanda Kingai Machi 28,2021, mwili huo ulitupwa usiku wa Machi 27, saa 5:30 usiku kutoka katika gari aina ya Toyota Noah ambayo namba zake hazikufahamika.

Hata hivyo katika maelezo yake, Kingai alieleza kuwa uchunguzi wa awali wa tukio hilo ni la mauaji na halikufanyika katika eneo hilo, bali waliotekeleza unyama huo walikwenda kumtupa katika eneo hilo.

Kamanda Kingai alieleza kulingana na madereva wa bodaboda waliokuwepo eneo hilo, gari hilo lilisimama kwa muda mfupi na kuwasha taa kisha kumtupa mtu ambaye baadaye alifahamika kuwa ni Blandina.

Kwa upande wa mdogo wa marehemu, Paulo Shaga alisema tayari suala hilo wameshaliachia jeshi la polisi kuendelea na uchunguzi ili waliofanya kitendo hicho waweze kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo husika. “

Suala hili liko mikononi mwa polisi na katika taarifa yao waliyoitoa awali walishaeleza kuwa wameanza uchunguzi ili kubaini waliohusika, sisi kama familia tunategemea taarifa kutoka polisi,” alisema Shaga.