Jeshi la Msumbiji limetangaza kuwa limeukomboa kikamilifu mji wa Palma wa fukwe za kaskazni mwa nchi hiyo katika mpaka wa Msumbiji na Tanzania. Mji huo ulitekwa na wanamgambo wanaojiita al Shabab, wiki moja iliyopita.
Redio ya taifa imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, watu wameshaanza kurejea katika makazi yao ili kuangalia madhara na wizi uliofanywa na wanamgambo hao. Redio hiyo pia imemnukuu msemaji mmoja wa jeshi la Msumbiji akisema kuwa, idadi kubwa ya wanamgambo wameuawa katika mapigano ya kuukomboa mji huo.
Makumi ya raia waliuawa na wengine wasiopungua 11,000 walikimbia makazi yao baada ya wanamgambo hao kuuvamia mji huo wa Palma mwishoni mwa mwezi uliopita wa Machi.
Mwandishi wa shirika la utangazaji la Uingereza BBC, Jose Tembe ameripoti kuwa, televisheni ya taifa ya Msumbiji imerusha hewani mkanda wa video unaoumuonesha mwanajeshi wa serikali akimfunika mfuko mweusi wa plastiki maiti mmoja katika mtaa mmoja wa mji wa Palma.
Shirika la habari la Ufaransa AFP limemnukuu msemaji wa jeshi la Msumbili, Brigedia Chongo Vidigal akisema kuwa, mji wa Palma na eneo la kuzalisha gesi yote yamekombolewa na sasa yako salama mikononi mwa jeshi la serikali.
Ijapokuwa taarifa zinasema kuwa baadhi ya wakazi wa mji huo wameanza kurejea, lakini mitaa ya Palma imeonekana mitupu. Televisheni ya BBC imeripoti kuwa, hospitali, mabenki na ofisi ya mwendesha mashtaka wa serikali yote yameharibiwa vibaya.
Taarifa hiyo imesema pia kuwa, Mkuu wa Mkoa wa Cabo Delgado, Valgy Tauabo ameutembelea mji wa Palma na kuwaahidi wakazi wake kuwasaidia kuujenga upya.
Credit:Parstoday