Misri na Sudan zimekataa pendekezo la Ethiopia la kushirikiana kwenye takwimu za shughuli za bwawa lake kubwa la umeme wa maji baada ya mazungumzo kati ya nchi hizo tatu kumalizika bila mafanikio. 

Kupitia mtandao wa Twitter, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia ilikuwa imezialika Sudan na Misri kushiriki katika kuteua waendeshaji wa bwawa kwa ushirikiano wa data kabla ya bwawa hilo kuanza kujazwa katika msimu wa mvua. 

Lakini serikali za Misri na Sudan zimesema zinatafuta makubaliano ya kisheria juu ya shughuli za bwawa hilo, huku zikipendekeza Umoja wa Ulaya, Marekani na Umoja wa Mataifa kuingilia kadhia hiyo. 

Ethiopia inasema inataka kutumia mradi wa umeme wa bwawa hilo kubwa kuinuwa uchumi wake, huku Misri na Sudan zikihofia athari za mradi huo kwa Mto Nile unaotegemewa na nchi hizo kama chanzo chao kikuu cha maji.