Na. Saidina Msangi na Josephine Majura, WFM, Dodoma

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb), amemuagiza Mhasibu Mkuu wa Serikali pamoja na Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali kuwasimamia ipasavyo wataalamu wa kada ya uhasibu nchini ili kukomesha kasoro za kiuhasibu na upotevu wa fedha za umma unaobainishwa kila mara na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Mhandisi Masauni alitoa maagizo hayo jijini Dodoma wakati wa utiaji Saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) na Bodi ya Uhasibu ya Kimataifa (ACCA) kwa ajili ya kuanzisha mafunzo ya uhasibu wa ngazi ya kimataifa ACCA katika vituo vya chuo hicho kwenye mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Dodoma.

“Taarifa ya CAG imeonesha udhaifu wa kimahesabu kwenye baadhi ya Taasisi za Serikali na Halmashauri jambo ambalo halikubaliki, sisi wadau wa sekta ya fedha tuna kazi kubwa ya kuendelea kukemea na kuwaelimisha wataalamu wa kada ya uhasibu na wakaguzi katika kutimiza majukumu yao ili kuwaletea wananchi maendeleo”, alisema Mhandisi Masauni.

Aidha, Mhe. Mhandisi Masauni alikipongeza chuo hicho kwa kupewa ithibati ya kuwa Kituo cha Mafunzo ya Uhasibu wa Kimataifa na kuratibu mitihani ya Taasisi ya ACCA itayowezesha chuo hicho kuratibu mafunzo hayo nchini.

“Ni furaha yetu kuona sasa tutaweza kuzalisha wataalamu wengi zaidi wa uhasibu wa kimataifa kupitia Chuo chetu cha Uhasibu Arusha, pia chuo kitaweza kuongeza wigo wa kuanza kudahili wanafunzi kutoka nchi jirani”, alisema Mhandisi Masauni.

Alisema kuwa mpango huo utaongeza idadi ya wataalamu wenye sifa ya uhasibu wa kimataifa na itaokoa fedha nyingi zilizokuwa zinatumika kuwasomesha wataalamu nje ya nchi.

Mhe. Mhandisi Masauni aliongeza kuwa ni vizuri kuwajengea wataalamu uwezo wa kushindana kimataifa lakini pia kwenda sambamba na viwango vya kimataifa ambavyo hubadilika mara kwa mara kulingana na sayansi na teknolojia.

Naye Mhasibu Mkuu wa Serikali Bw. Francis Mwakapalila alisema kuwa kuanzishwa kwa kituo cha mafunzo na udahili wa mitihani ya ACCA (CPA kwa kiwango cha Kimataifa) kutaongeza wigo wa wataalamu nchini na hivyo kuboresha uandaaji wa taarifa za uhasibu.

“Ujuzi na maarifa yatakayopatikana yatakuwa ni nyenzo muhimu itakayoongeza ufanisi katika utendaji kazi na kuendeleza taaluma ya uhasibu na kuongeza idadi ya wataalamu”, alisema Bw. Mwakapalila.

Alitoa rai kwa wote walio katika Taasisi za umma na binafsi kuchangamkia fursa hiyo ili kupata weledi katika taaluma ya uhasibu na kuleta msukumo mkubwa wa kukuza uchumi nchini.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Prof. Eliamini Sedoyeka alisema kuwa makubaliano hayo yatasaidia wataalamu wa uhasibu kupata ujuzi na kutambulika kimataifa lakini pia kusaidia kutoa mafunzo kwa gharama nafuu.

“Baada ya muda mrefu sasa kumetokea mabadiliko mbalimbali katika sekta yetu hii na pia muingiliano wa masuala ya kimataifa. Lakini pia, umekuwa ni wakati mzuri wa kuhakikisha kuwa wataalam wetu wa uhasibu pia wanapata sifa za Kimataifa na kutambulika vyema katika ulimwengu tuliopo”aliongeza Prof. Sedoyeka

Naye mwakilishi wa Bodi ya Uhasibu ya Kimataifa (ACCA) Bw. Jenard Lazaro alisema kuwa chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kinachomilikiwa na Wizara ya Fedha na Mipango,  kinakuwa chuo cha tatu kwa nchi za Afrika ya Mashariki kutoa mafunzo hayo na kusisitiza ushirikiano katika utekelezaji wa makubaliano hayo ili kuendeleza fani ya uhasibu nchini.

Bodi hiyo ya ACCA yenye makao yake makuu nchini Uingereza ina wanachama wapatao laki mbili huku hapa nchini ikiwa na wanachama 400 na wanafunzi zaidi ya 2,000.

 Mwisho.