Na Steven Nyamiti, Kahama.
Imeelezwa kuwa, Wizara kupitia Tume ya Madini kupanga  bei elekezi ya kuuza madini Nchini umesaidia wauzaji na wanunuzi kuondoa ulanguzi wa bei, na kuchochea wachimbaji kuleta madini yao kwa wingi kwenye masoko ya madini Nchini.


Hayo yameelezwa na Kaimu Afisa Madini wa Mkoa wa Kimadini Kahama Fabian Itaru tarehe 17 April, 2021 katika ziara yake na wanahabari kutembelea Masoko ya Madini, Vituo vya ununuzi wa Dhahabu na maeneo ya machimbo ya Dhahabu wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga.


Ameeleza kuwa, kuanzishwa kwa masoko ya madini kumefanya Dhahabu yote kuingia kwenye mfumo wa soko na malipo halali ya Serikali kukusanywa kwa wakati.


"Kuanzishwa kwa masoko haya kumeongeza mapato kwa Serikali. Ofisi ya madini kipindi cha nyuma ilikuwa inapewa lengo la kukusanya bilioni 45 kwa Mwaka ambapo kabla ya kuanzishwa masoko hayo Mwaka 2016 hatukuwahi kufikia lengo, lakini baada ya kuanzishwa masoko ya madini malengo ya Ofisi ya Madini Kahama kupitia Tume ya Madini yamefikia lengo.Mwaka huu tumepangiwa kukusanya bilioni 79 ambapo hadi sasa tumekusanya bilioni 72 sawa na wastani wa asilimia 91" ameeleza Itaru


Amefafanua kuwa, Makusanyo hayo yametokana na masoko ya Madini, shughuli nyingine za Wachimbaji wadogo, Kodi za leseni zinazolipwa, mrabaha na ada za ukaguzi zitokanazo na uzalishwaji wa Dhahabu Kahama.


Naye, Mjiolojia Samuel Baruti kutoka Tume ya Madini akizungumza Katika kituo cha Ununuzi Madini Mwime Kahama, amewaeleza wanahabari kuwa, huko nyuma hali ilikuwa ngumu Sana kwa wachimbaji wadogo kabla Serikali haijaanzisha utaratibu wa masoko.


Amesema kulikuwa na watu wanafanya biashara mitaani na kujipangia bei tofauti na kipindi hichi ambacho Serikali inapanga bei elekezi ili mchimbaji mdogo aweze kuona faida ya uchimbaji wake.


Ameeleza kuwa, miaka ya nyuma mfaidika mkubwa alikuwa mfanyabiashara wa madini lakini baada ya kuanzisha mfumo wa masoko umefanya  wafanyabiashara kukusanyika eneo moja katika soko la madini.


Kwa Upande Meneja  wa Umoja  wa Kwenye Mashamba  Ilindi  Mwime Joseph Nalimi, akieleza kwa niaba ya wachimbaji wadogo Mwime ameiomba wizara kuwasaidia  wachimbaji wadogo ili  waweze kukopesheka na kupata udhamini wa mabenki, kutengeneza miundombinu ya machimbo ya Mwime, na kupata ripoti ya kijiolojia ya maeneo yao ili waache kuchimba kwa kubahatisha.


Nalimi, ameishukuru ofisi ya madini Mkoa wa Kimadini Kahama kwa kuanzisha vituo vya uuzaji na ununuzi Dhahabu karibu na maeneo ya machimbo ambavyo vimesaidia kupata soko la uhakika la Dhahabu