Mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota, ameiomba serikali kuanza kutekeleza mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma na Liganga ili Bandari ya Mtwara ifanye kazi kwa ufanisi.

Akichangia leo bungeni bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2021/22, Chikota amehimiza matumizi ya bandari hiyo kutokana na serikali kufanya uwekezaji mkubwa uliogharimu zaidi ya Sh.Bilioni 57.

“Bandari ya Mtwara ina uwezo wa kupokea tani milioni moja naomba ule mradi sasa wa kujenga reli kutoka Mtwara hadi Mbambabay na mradi wa Mchuchuma na liganga sasa uanze ili utumike ipasavyo,”amesema.

Kuhusu zao la korosho, Chikota ameomba Wizara ya Kilimo kurekebisha dosari zilizopo katika mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kuwa umeleta mafanikio makubwa sana kwenye sekta ya korosho.

Pia, ameitaka serikali ijipange kutumia maji kutoka mto Ruvuma kupeleka Mtwara ili kuondoa tatizo la maji.