WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea kiwanda kuunganisha magari cha GFA kilichoko Kibaha mkoani Pwani na ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wawekezaji wote kwamba Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano.

”Nimeridhishwa na kufarijika kuona hali ya kazi inayofanyika kiwandani hapa, niwahakikishie kwamba Serikali itaendelea kuwaunga mkono katika uwekezaji wenu. Mheshimiwa Rais aliona kazi yenu kupitia mitandao na akanituma nije nione”.

Waziri Mkuu ametembelea kiwanda hicho leo (Jumatatu, Aprili 19, 2021). Amesema hayo ndiyo mawazo ya viongozi wa nchi tangu Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Pombe Magufu na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

”Mmewekeza kwa wakati sahihi na kwenye nchi sahihi na uwekezaji huu lazima utawaletea faida kwa sababu sera zetu za uwekezaji ni sahihi. Niwahakikishie kwamba Serikali yetu imejipanga vizuri katika kuwahudumia wawekezaji”.

Pia, Waziri Mkuu ameupongeza uongozi wa mkoa wa Pwani kwa kutumia vizuri fursa ya maendeleo ya viwanda nchini kwa kutenga ardhi ya kutosha kwa ajili ya uwekezaji katika Halmashauri zake zote.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka Watanzania waendelee kuiunga mkono na kuiamini Serikali yao. Pia, Waziri Mkuu amewataka Watanzania walioajiriwa na kampuni hiyo wafanye kazi kwa bidii na wawe waaminifu na waadilifu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo amesema mkoa huo katika kipindi cha kuanzia 2015 hadi 2021 umejenga viwanda 1,100 na kufanya mkoa huo kuwa na viwanda 1,438 kati yake vikubwa ni 82 kikiwemo na cha GFA. “Viwanda hivi vimetoa ajira za moja kwa moja 50,000 na za muda 100,000”

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa GFA, Bw. Jawaad Karmali alisema kiwanda chao kina uwezo wa kuunganisha magari ya aina yote kutokana na teknolojia waliyo nayo ila kwa sasa wameanza kwa kuunganisha malori.

Alisema kiwanda chao kimeajiri watumishi takribani 100, huku uwekezaji wao ukigharimu sh. bilioni 12. Uwekezaji huo unafanyika kwa awamu mbili, ambapo katika awamu ya kwanza wameshatumia sh. bilioni nne.

(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,