Zaidi ya watu 75 wamefariki dunia na wengine wengi wahawajulikani waliko baada ya mafuriko na maporomoko ya ardhi kuyakumba baadhi ya maeneo nchini Indonesia na Timor Mashariki, maafisa wa eneo hilo wameisema leo Jumatatu.

Mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa yamesababisha maafa katika maeneo kati ya Flores, chini Indonesia na Timor ya Mashariki, na kusababisha maelfu ya watu kukimbilia katika vituo vya mapokezi.

Mvua hiyo imesababisha mabwawa kujaa maji na kusababisha mafuriko katika maeneo ambapo maelfu ya nyumba zimeharibika, wakati waokoaji wamekuwa wakijitahidi kutoa msaada kwa waathiriwa.

"Kuna watu 55 wamefariki dunia, lakini idadi hii inaendelea kubadilika, kwani watu 42 bado hawajulikani waliko," amesema Raditya Djati, msemaji wa Idara ya majanga na usaidizi wa kibinadamu nchini Indonesia kwenye televisheni ya MetroTV.

Takriban watu 21 wameuawa katika Timor Mashariki, kulingana na afisa wa Timor. Vifo vingi vilitokea katika mji mkuu wa Dili.

Mashariki mwa kisiwa cha Flores cha Indonesia, nyumba nyingi, barabara na madaraja vilifunikwa na matope, na kufanya hali kuwa ngumu kwa waokoaji kujaribu kufikia maeneo yaliyoathiriwa zaidi.

Credit:RFI