Kwa mara nyingine madaktari wa mpinzani wa Rais Vladimir Putin, aliyefungwa gerezani, Alexei Navalny wamezuliwa kumuona mpinzani huyo licha ya kuongezeka kwa wasiwasi wa kuzorota kwa afya yake.

Timu ya madaktari akiwemo na daktari binafsi wa Navalny Anastasia Vasilyeva walikwenda katika gereza jipya alikohamishiwa mpinzani huyo lakini walizuiliwa kumuona. Hata hivyo waliambiwa wajaribu tena baadae.

Tangu mwanzoni mwa mwezi huu, timu ya madaktari imekuwa ikifanya jitahda za kumuona Navalny mwenye umri wa miaka 44, baada kuanza kufanya mgomo wa kula Machi 31 akishinikiza matibabu bora kutokana na maradhi yanayomsumbua.

Mwishoni mwa juma madaktari wake walionya kwamba afya yake inazorota kwa kasi, na anaweza kupoteza maisha dakika yoyote, kauli ambayo imeifanya Marekani iitishie Urusi kuichukulia hatua iwapo atafariki.