Vijana nchini wameshauriwa kujiunga katika vikundi na kuanzisha mashamba yanayotumia kilimo hai kwa kulima bila kutumia kemikali ili kuwa na uhakika wa soko na kipato.

Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa Mkakati wa Vijana Kushiriki katika kilimo toka Wizara ya Kilimo Revelian Ngaiza jana (27.04.2021) wakati alipotembelea vikundi vya vijana wanaofanya kazi za kilimo hai kijiji cha Kalengakelu wilaya ya Mlimba Mkoa wa Morogoro.

Ngaiza aliongozana na wataalam wa shirika la Kilimo Endelevu (Sustainable Agriculture of Tanzania-SAT) alijionea mashamba ya mpunga ya vijana wa kijiji cha Kalengaleku ikiwemo vitongoji vya Nyumbanguru na Samola ambao wanazalisha mazao ya mpunga na mazao ya bustani kwa njia ya kilimo hai.

"Lengo la Wizara ya Kilimo ni kuona nguvu kazi iliyopo ya vijana takribani asilimia 58 inashiriki kwenye kazi za uzalishaji mali kupitia kilimo ili kukuza uchumi wa kaya na taifa" alisema Ngaiza

Mratibu huyo wa Mkakati wa Vijana katika kilimo alibainisha fursa zilizopo kwenye kilimo ikiwemo kilimo hai ambacho hakitumii kemikali kuwa ni uhakika wa masoko kutokana na watum wengi kupenda kutumia vyakula vilivyozalishwa bila kemikali 

Naye Mratibu wa mradi wa Kilimo Hai toka shirika la SAT  wilaya ya Mlimba Elizabeth Msobi alisema jumla ya vijana 97 kwenye kijiji cha Kalengakelu wamejiunga kwenye vikundi na wanazalisha mazao ya mpunga na bustani kwa njia ya kilimo hai (organic farming) bila kutumia kemikali au madawa kuua wadudu hivyo kutunza mazaingira na afya ya mlaji.

Msobi aliongeza kusema changamoto kubwa kwa vijanwa Mlimba ni ukosefu wa ardhi hali inayokatisha tamaa vijana wengi kujiunga hususan wanawake  .

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi cha Kilimo Hai Kitongoji cha Samola kijiji cha Kalengakelu Daud  Kalinga aliomba serikali iagize viongozi wa vijiji kugawa ardhi kwa vijana.

"Serikali itupatie ardhi sisi vijana ili tulime Kilimo hai badala ya sasa tunachangishana kukodi ekari moja kwa shilingi 100,000 ni fedha nyingi mno,tunashindwa kufanya kilimo" alisema kijana Daudi.