Kansela Angela Merkel amewataka watu wa Ujerumani kukubaliana na hatua mpya zilizochukuliwa na serikali na ambazo zinatumika nchini kote. 

Merkel amesema kwa kuzingatia yanayotokea kwenye nchi zingine za Ulaya kuhusiana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona, serikali yake haikuwa na njia nyingine mbadala ila kuweka sheria mpya ya kutotoka nje usiku iliyoanza kutumika kote nchini Ujerumani hapo jana Jumamosi. 

Bibi Merkel amezitolea mfano nchi za Uingereza, Ureno na Ireland amesema zimefaulu kupunguza idadi ya watu wanaoambukizwa kutokana na kuweka vizuizi vikali kwa ajili ya kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona. 

Hapa nchini Ujerumani pamoja na amri ya kutotoka nje kuanzia saa nne usiku hadi saa 11 alfajiri, sheria nyingine zinahusu kupunguza idadi ya watu kukutana na kufungwa kwa maduka ya bidhaa zisizo za muhimu. 

Kansela Merkel amesema kwenye hotuba yake ya kila wiki kwa njia ya video kwamba kanuni hizo mpya ni ngumu lakini zinatakiwa kutekelezwa ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona nchini Ujerumani.