Serikali ya nchini Myanmar imetanuwa kampeni yake ya kuwaandama wapinzani wa mapinduzi ya kijeshi ya Februari Mosi, kwa kuchapisha majina ya wasanii na watu mashuhuri wanaounga maandamano dhidi ya serikali hiyo. 

Majina ya watu hao yaliyochapishwa jana na leo kwenye gazeti la Global New Light linalomilikiwa na jeshi, yanajumuisha waigizaji, wanamuziki na watumiaji wa mitandao ya kijamii ambao wana wafuasi wengi. 

Jeshi linasema watu hao mashuhuri wanavunja sheria ya uhalifu kwa kusambaza habari zinazochafua amani na utulivu wa nchi. 

Licha ya jeshi kuuwa zaidi ya waandamanaji 550 tangu lichukuwe madaraka kwa nguvu mwanzoni mwa mwezi Februari, wananchi wamekuwa wakiingia kila siku mitaani kupinga utawala huo. 

Jana Jumatatu, maelfu ya waandamanaji walitumia ishara ya kupiga makofi nchi nzima kuwashukuru wenzao waliopoteza maisha kwenye miezi miwili ya maandamano.