Iran imekataa kukutana ana kwa ana na Marekani, wakati wa mkutano na washirika waliosalia kwenye makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 mjini Vienna wiki ijayo. 

Naibu Waziri wa Mambo ya Kigeni Abbas Araqchi amenukuliwa kupitia tovuti ya wizara hiyo kwamba Marekani haitahudhuria kikao chochote ambacho Iran itashiriki, ikiwa ni pamoja na mkutano wa pamoja wa tume ya mkataba huo wa nyuklia na kuongeza kuwa hilo liko wazi. 

Wanadiplomasia wamesema maafisa wa Tehran na Washington wataenda Vienna wiki ijayo ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuufufua mkataba huo kati ya Iran na mataifa makubwa ulimwenguni ingawa hawatafanya mazungumzo hayo ya ana kwa ana. 

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Heiko Maas amesema ilikuwa ni hatua nzuri kwa mazungumzo hayo kurejea na kuongeza kuwa iwapo mkataba huo utaanza kutekelezwa tena kikamilifu itakuwa ni hatua nzuri ya nyongeza kuelekea usalama wa kikanda na majadiliano ya masuala mengine ya ustahimilivu wa kikanda.