Serikali ya Indonesia imekiri kuvutiwa na fursa za uwekezaji zilizopo katika Mkoa wa Songwe, hususani kwenye sekta za kilimo, Madini, Biashara na Bandari kavu, ambapo imeonyesha nia ya kutaka kuwekeza katika maeneo hayo.

Balozi wa Indonesia Nchini  Profesa Ratlan Pardede amebainisha  Mei 29 katika ziara yake ya siku mbili mkoani hapa kwa lengo la kutembelea na kujionea fursa za uwekezaji zitakazowezesha kupatikana manufaa ya kiuchumi kati ya Tanzania na Indonesia kupitia Mkoa wa Songwe.

Profesa Pardede ambaye pia ni mwakilishi wa nchi hiyo katika nchi za Burundi, Rwanda na Comoro, alitaja miradi na maeneo ambayo wao wameyaona kama fursa ya uwekezaji kuwa ni eneo la kilimo, ambapo nchi hiyo itawezesha ujenzi wa viwanda vya kuchakata chakula cha mifugo.

"Kama mlivyoonyesha katika taarifa yenu iliyowasilishwa hapa leo kuhusu kilimo, katika eneo hili tumebaini kuna fursa kubwa ya uwekezaji wa viwanda vya kuchakata chakula cha mifugo ili kuongeza tija kwa wakulima.", amesema Profesa Pardede.

Ametaja maeneo mengine kuwa ni mpaka wa Tunduma kati ya Tanzania na Zambia ambao ni lango la nchi za Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika(SADC) kuwa kuna fursa kubwa ya biashara, ambapo wanalenga kufungua maduka makubwa (Shoping Mall) ambayo yatakuwa na bidhaa za indonesia ikiwa ni pamoja na ujenzi wa bandari kavu.

Katibu Tawala Mkoa wa Songwe Dkt. Seif Shekalaghe aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa amesema ziara hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwa mkoa wa Songwe ambao ni mzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula.

"Tumeona fursa ya wakulima wetu kufanya biashara ya kuuza maparachichi ambayo yanazalishwa kwa wingi hapa kwetu, lakini pia zao la soya ambalo soko lake ni kubwa katika nchi ya Indonesia.", Amesema Dkt. Shekalaghe.

Kwa upande wake, Mwenyekiti waWenye Viwanda, wafanyabiashara na wakulima (TCCIA) Songwe Mkoa wa Songwe, Charles Chenza amesema wanatarajia kutumia fursa hiyo ya ushirikiano wa nchi hizi mbili katika kuimarisha biashara ya bidhaa za kilimo.

Balozi Profesa Pardede ameongozana na Naibu Balozi wa nchi hiyo, Wahono Yulianto, pamoja Ofisa wa mambo ya nje kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Luangisa Emmanuel ambao wamefanikiwa kutembelea Wilaya za Ileje, Mbozi na Halmashauri ya Mji Tunduma.