Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa idadi ya waliofariki kutokana na virusi vya corona nchini India imepindukia watu laki mbili siku ya jana. 

Hii ni baada ya zaidi ya watu elfu tatu wengine kufariki katika kipindi cha saa ishirini na nne zilizopita hiyo ikiwa ni rekodi ya vifo kwa siku moja. 

Kwa sasa India imesajili visa milioni 18 vya maambukizi na katika masaa ishirini na nne yaliyopita watu 360,000 wameambukizwa virusi vya corona. Mwezi huu wa Aprili pekee, nchi hiyo imeshuhudia maambukizi milioni sita. 

Mlipuko huo wa maambukizi ambao unadaiwa kutokana na aina mpya ya kirusi pamoja na mikutano mikubwa kisiasa na kidini, imesababisha hospitali kulemewa na ukosefu wa vitanda, dawa na gesi muhimu ya oksijeni. 

India kufikia sasa imewachoma chanjo watu milioni 150 na kuanzia Jumapili, mtu yeyote aliye na umri wa miaka 18 au zaidi ataruhusiwa kupokea chanjo.